Mark 4

Mfano Wa Mpanzi

(Mathayo 13:1-9; Luka 8:4-8)

1 aIsa akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umekusanyika kumzunguka ulikuwa mkubwa, kiasi kwamba ilimbidi Isa aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari. 2 bAkawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema: 3 c“Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. 4Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. 6Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao. 8 dMbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”

9 eKisha Isa akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Sababu Za Mifano

(Mathayo 13:10-17; Luka 8:9-10)

10 fAlipokuwa peke yake, watu waliokuwepo naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake. 11 gNaye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano, 12 hili, “ ‘daima waone lakini wasitambue,
daima wasikie lakini wasielewe;
wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

Isa Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

(Mathayo 13:18-23; Luka 8:11-15)

13Kisha Isa akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine? 14 iYule mpanzi hupanda neno. 15 jHawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao. 16Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha. 17Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani. 18Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; 19 klakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae. 20Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano Wa Taa

(Luka 8:16-18)

21 lAkawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake? 22 mKwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni. 23 nMwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

24 oNaye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi. 25 pKwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Mfano Wa Mbegu Inayoota

26 qPia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27 rAkiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo. 28Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke. 29 sLakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia, maana mavuno yamekuwa tayari.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

(Mathayo 13:31-32, 34; Luka 13:18-19)

30 tAkawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza? 31Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. 32 uLakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye matawi yake.”

33 vKwa mifano mingine mingi kama hii Isa alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa. 34 wHakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Isa Atuliza Dhoruba

(Mathayo 8:23-27; Luka 8:22-25)

35 xSiku hiyo ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni twende mpaka ng’ambo.” 36 yWakauacha ule umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye. 37Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. 38Isa alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

39Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

40 zIsa akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

41Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”
Copyright information for SwhKC